Historical Background of Tanzania Broadcasting Corporation (TBC)

Sauti ya Dar es Salaam

Wasanii wakiwa studio za Sauti ya Dar es Salaam miaka ya 1950.

Before Independence

1951: Sauti ya Dar es Salaam ilianzishwa

Mwezi Machi 1955, Sauti ya Dar es Salaam ilibadilishwa hadhi na kuwa idara kamili ya serikali iliyopewa jina la Tanganyika Broadcasting Services (TBS). Kwa pesa za ufadhili utangazaji ulipanuliwa kufikia maeneo mengi ya nchi na makao makuu mapya yalianzishwa baadaye Pugu Road, Dar es Salaam (Sasa inajulikana kama Barabara ya Julius K. Nyerere). TBS ilipatiwa ofisi chache, studio mbili, chumba cha uongozaji, maktaba ndogo ya rekodi, na kifaa cha kurekodi simu. Ilitumia transimita ya mawimbi mafupi ya Marconi kW 20, ambacho kilikuwa na nguvu zaidi katika Afrika ya Mashariki wakati huo, TBS ilisikika karibu eneo lote la nchi, pia ilisikika nchi mbali kama Japani, Ufini, na Nyuzilandi. Matangazo ya TBS yalikuwa hewani kwa saa nane. Wakati wa mihula ya shule, vipindi vya elimu vilitangazwa kutoka saa mbili unusu hadi saa nne unusu asubuhi.

1955: Sauti ya Dar Es Salaam ilibadilishwa jina na kuitwa Tanganyika Broadcasting Services

Mnamo Februari 1956, mwanachama wa Huduma za Jamii aliwasilisha kwenye Baraza la Kutunga Sheria mswada wa shirika kuchukua madaraka ya huduma ya utangazaji. Alisisitiza kuwa itakuwa huru na haitaonekana kama chombo au mdomo wa Serikali. Katika mjadala uliofuata mjumbe mmoja aliuliza kama inaweza kuhamishiwa Dodoma katika ya nchi na mwingine alisisitiza haja ya kudhibiti uhariri sahihi na tahadhari juu ya kuanzishwa kwa utangazaji wa kibiashara. Tarehe 1 Julai, 1956, TBS ilibadishwa na kuwa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC). TBC ilikuwa shirika la umma kwa kufuata mtindo wa BBC. Hata hivyo uhuru wa kujiendesha na kujitawala ulibinywa kwa sababu ililazimika kufanya kazi na kufuatiliwa kwa karibu sana na serikali ya Kikiloni na kufanya kazi kama msemaji wa Serikali ya Kikoloni.

1956: Jina la Tanganyika Broadcasting Services lilibadilishwa na kuwa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC)

Mnamo 1957, ruzuku ya Pauni 20,000 kutoka Mfuko wa Maendeleo na Ustawi wa Kikoloni na Ustawi (Colonial Development and Welfare Fund) ilipitishwa kwa ajili ya kupata transimita ya pili ya mawimbi mafupi (kw 10) na transimita nyingine ya mawimbi ya wastani (kw1¼). Kiasi cha Pauni 5,000 kinachohitajika kununua vifaa vipya kilitolewa na utawala. Jumla ya muda wa kurusha matangazo uliongezwa kutoka saa 27 hadi 37 kwa wiki. Takriban 70% ya vipindi vilitangazwa kwa Kiswahili. TBC ilitoa habari za ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya BBC yenye makao yake jijini London ambayo ilikuwa imezinduliwa tarehe 27 Juni 1957. Habari za kila siku za ndani kwa lugha ya Kiingereza zilipatikana kutoka gazeti la Tanganyika Standard.

Mnamo Mei 1958, Thomas W. Chalmers, afisa wa BBC, aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kwanza wa utangazaji. Chalmers, hapo awali alihusika kuendeleza Shirika la Utangazaji la Nigeria (NBC), akawa mtendaji mkuu wa bodi. Tangu mwanzo, mkurugenzi alijitahidi kuhakikisha uhuru wa kisiasa wa TBC kwa kujaribu kuvutia matangazo ya biashara. Ingawa matangazo ya biashara yalianza kukubaliwa mwaka wa 1955, kituo bado kiliendeshwa kwa ruzuku ya serikali. Awali, shirika lilikuwa makini kufikia uwiano wa maoni wakati mada zenye utata zikijadiliwa. Lakini sera hii ilikuja kuwa chini ya shinikizo la serikali ili mijadala ya umma iendelee kwenye redio masuala fulani yakawa na ukomo zaidi.

Tarehe 1 Julai 1960, TBC ilianzisha huduma yake ya habari, na Tanganyika Standard haikusambaza tena matangazo kwa kituo hicho ingawa TBC iliendelea kununua habari kutoka gazeti hilo kwa misingi ya uwakala. Kwa ripoti za kimataifa, TBC iliendelea kutegemea vipindi vya BBC katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili. Hadi kufikia uhuru, matangazo ya redio katika nchi ya Tanganyika yalikuwa tayari yana matokeo ya kushangaza. Kwanza, visambaza sauti vitatu vya mawimbi mafupi ziliwezesha matangazo kupatikana karibu nchi nzima, na visambaza sauti viwili vya mawimbi ya kati zilihudumia Dar es Salaam na maeneo yake ya jirani. Pili, watu 94 kati ya 123 walioajiriwa na kituo walikuwa Waafrika waliofunzwa vyema na wenye uzoefu wa uendeshaji wa mfumo wa utangazaji.

Mwaka wa 1959, vifaa vya ziada, transimita ya mawimbi mafupi ya kW 10 na transimita ya mawimbi ya kati cha 1 ¼ kW, ziliongezwa. Kama matokeo ya uboreshaji huo, TBC iliweza kutangaza idhaa mbili kwa wakati mmoja - Idhaa cha Taifa kwa Kiswahili na idhaa ya pili kwa wasikilizaji wanaozungumza Kiingereza. Idhaa ya kwanza ilikuwa hewani asubuhi kutoka saa kumi na mbili na robo hadi saa mbili, mchana kutoka saa sita kamili hadi saa saba unusu, na jioni kutoka saa kumi unusu hadi saa nne na robo usiku. Idhaa ya pili, ambayo hasa ilitegemea kanda zilizorekodiwa na vyanzo vya nje kuhusu habari za Kitanzania, ilirusha matangazo yake kuanzia saa kumi na mbili kamili hadi saa mbili kamili asubuhi na kutoka saa moja jioni hadi saa nne na robo usiku. Zaidi ya hayo, kituo kilitangaza programu za kila siku kwa ajili ya wasikilizaji wa Kiasia kutoka saa kumi na mbili unusu mpaka saa moja jioni, matangazo hayo yalikuwa kwa lugha ya Hindustani na Gujerati.

Januari 1962, Mikidodi B. Mboe alimrithi Thomas Chalmers kama mkurugenzi wa utangazaji. Miongoni mwa matukio maarufu wakati wa Mboe ni kuanzishwa kwa Idhaa ya External Service na Idhaa ya tatu. Idhaa ya External Service iliyokuwa inarushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam ilianzishwa mahususi kusaidia harakati za kupigania uhuru katika Rhodesia (sasa Zambia na Zimbabwe) na Nyasaland (sasa Malawi). Programu hii ilikuwa hewani kila siku kuanzia saa mbili kamili usiku hadi nne kamili usiku.

Mwezi Machi 1964, matangazo ya Rhodesia na Nyasaland yalibadilishwa na programu ya ukombozi wa Afrika Kusini na Afrika Kusini Magharibi (sasa Namibia). Ili kuongeza ufikiaji, iliongezwa transimita ya 100 kW kutoka China. Viongozi wa wapigania uhuru katika nchi hizo waliishi na kuratibu harakati za ukombozi katika nchi zao kutokea Tanzania ambapo walirusha matangazo ya redio ya kuhamasisha wananchi wao kushiriki katika mapambano hayo kupitia idhaa hiyo ya External Service. Mnamo Januari 1968, harakati nane za ukombozi, ikiwa ni pamoja na FRELIMO na SWAPO, walikuwa wakichangia urushaji wa matangazo ya redio katika lugha za Kiafrikaans, Kiingereza, Herero, Ndebele, Nyanja, Ovambo, Kireno, na Shona. Baada ya nchi za Kusini mwa Afrika kupata uhuru, Idhaa ya External Service haikuendelea kurusha matangazo yake. Idhaa ya tatu pia ilianza shughuli zake mnamo 1962 na ililenga kuelimisha hadhira kwa kutangaza vipindi vya kielimu zaidi. Utangazaji wake ulikuwa hewani siku za wiki kutoka saa kumi na moja kamili hadi saa moja kamili jioni.

RTD Tanzania

Bango la Radio Tanzania Dar es Salaam.

Mwaka 1965 Serikali ya kizalendo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipeleka Bungeni mswada wa kuvunjwa kwa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ilianzishwa kama idara ya Wizara ya Habari, Utangazaji na Utalii. Baada ya matangazo ya redio kuenea kulikuwa na shinikizo la kuongeza matangazo ya redio katika baadhi ya lugha za makabila, lakini Nyerere alikataa. Badala yake, RTD ilitumika kama njia ya kueneza Kiswahili kote nchini. Matangazo ya lugha ya Kiingereza yalifutwa mwaka 1970, Tanzania ikawa nchi pekee ya Kiafrika inayotumia lugha moja tu katika redio yake (Kiingereza bado kinatumika katika stesheni ya TBC International). Muda wa matangazo ya kila siku uliongezeka hadi Saa 6 ¼ mnamo Septemba 26, 1970. Serikali iliona redio kama njia yao bora ya kuunganisha vijiji na serikali na kuwahamasisha watu kujivunia nchi yao na kujaribu kuifanya kuwa bora zaidi. Uingizaji wa televisheni ulipigwa marufuku na sheria ya mwaka wa 1974, baraza la mawaziri la serikali ya Julius Kambarage Nyerere lilipinga kuanzishwa kwa televisheni, likisisitiza kuwa televisheni hiyo ilikuwa ghali sana na kwamba utangazaji wa redio Tanzania bado haujakamilika. Hadi mwaka 1994, hapakuwa na matangazo yoyote ya televisheni yanayofanya kazi Tanzania Bara. Kituo pekee kilikuwa Televisheni ya Zanzibar (TVZ). TVZ ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuingia mkataba na kampuni ya Uingereza kuanzisha kituo kisiwani humo.

RTD Tanzania

Waandishi na wanahabari wa Redio Tanzania Dar es Salaam walipokwenda kumuaga Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Ikulu Dar es Salaam alipotangaza kustaafu mwaka 1985.

Mipango ya kuzindua kituo cha televisheni Tanzania bara ilifufuliwa mwaka wa 1985 wakati serikali ilipounda Kikosi Kazi cha Televisheni ambacho kilikuwa chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Posta na Mawasiliano Tanzania (TPTC), F. C. Kasambala. Ripoti ya mwisho ya kikosi kazi iliyowasilishwa mnamo Oktoba 1989 ilisema mazingira yanaruhusu kuanzisha kituo cha televisheni na hivyo, ufungaji wa teknolojia hiyo unapaswa kuendelea haraka. Lakini kamati hiyo ilipoanza kuulizia gharama kutoka kwa taasisi za kimataifa ilionyesha ni ghali sana, kwa mfano, makadirio ya kwanza ya teknolojia ya upitishaji wa satelaiti yalifikia dola za Marekani bilioni moja. Tarehe 13 Oktoba 1989, gazeti la Business Times lilichapisha makala iliyodai: “Kwa Dola za Marekani milioni 7 tu ... Tanzania inaweza kuwa na TV.“ Siku chache tu baada ya makala ya Business Times kuchapishwa, mnamo Novemba 6, 1989, wakati huo Waziri wa Habari na Utangazaji, Hassan Diria, aliteua Kamati ya Ushauri ya Kiufundi ya Televisheni ambayo iliongozwa na Ambrose Ottaru. Baadaye, tarehe 12 Aprili 1990, kamati ilikabidhi ripoti yake kwa Diria. Ripoti hii ilipelekea kuwekwa kwa mikakati ya kukamilisha uanzishwaji wa kituo cha televisheni ifikapo mwaka 2000. Serikali ilianza kufanya majaribio ya huduma za matangazo ya Televisheni ya Taifa (TVT) tarehe 16 Oktoba 1999 na matangazo rasmi yakaanza terehe 15 Machi 2000. Tarehe 1 Julai, 2007 Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na Televisheni ya Taifa (TVT) ziliunganishwa na kuwa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC).

Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), serikali ilianzisha mpango wa kupanua usikivu maeneo yote nchini ambapo usikivu uliongezeka kutoka wilaya 87 mwaka 2017 sawa na asilimia 54 ambapo hadi Machi 2019 wilaya 102 zilifikiwa na matangazo ya redio ambayo ni sawa na asilimia 63. Julai 26, 2021, UCSAF kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ilizindua kituo cha kurushia matangazo ya TBC Taifa na TBC FM mkoani Dodoma, kituo kama hicho kimejengwa pia katika mkoa wa Arusha na Morogoro kuboresha usikivu wa redio katika maeneo mbalimbali nchini. Agosti 3, 2021, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liliingia mkataba wa miaka 10 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa haki za kurusha matangazo ya redio ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia msimu wa 2021/2022. Mkataba huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 3.54 unaipa TBC haki ya kurusha matangazo kwa sauti lakini hauvifungi vyombo vingine vya habari kurusha matangazo ya ligi kuu isipokuwa kwa makubaliano rasmi kati yao na TBC na TFF. Aprili 14, 2022, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua vituo vinne vya kuongeza usikivu wa redio za TBC Taifa na TBC FM vilivyopo Ruangwa (Lindi), Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera), tukio la uzinduzi limefanyika Ruangwa mkoani Lindi. Vituo hivyo vilijengwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).