Jumatano, 11 Juni 2025, 04:33:44
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Ukweli na Uhakika
TBC Logo

Shirika la Utangazaji Tanzania lina historia ndefu sana ikianzia baada ya Redio SAUTI YA DAR ES SALAAM iliyoanzishwa tarehe 01 Julai, 1951, ikirusha matangazo yake kwa Kiswahili mara moja kwa wiki.

Mwaka 1955 Sauti ya Dar es salaam iliyokuwa na makao yake katika mtaa wa Kichwele ilibadilishwa na kuwa Tanganyika Broadcasting Services (TBS) na kuhamia Pugu Road, sasa Barabara ya Nyerere. TBS ilipata umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na matangazo yake, ilipokea habari kutoka Japan, Finland na New Zeland.

Mnamo tarehe 01 Julai, 1956 TBS ilibadilika na kuitwa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC). Baada ya juhudi za kupigania uhuru wa Tanganyika na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, TBC ilibadilishwa jina na kuitwa Redio Tanzania Dar es salaam (RTD), tarehe 01 Julai, 1965. RTD ilitumika kuhamasisha na kutoa elimu juu ya Azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ilikuwa na idhaa tatu ambazo ni idhaa ya Taifa, idhaa ya biashara na idhaa ya kiingereza (External Services of Redio Tanzania Dar es salaam).

Katika kuboresha ubora wa vipindi na kuimarisha utangazaji kwa vyombo vya serikali, mnamo tarehe 12 Juni, 2004 iliundwa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT) ambayo iliunganisha Redio Tanzania Dar es salaam na Televisheni ya Taifa (TVT). Hii ilisaidia kufanya vyombo hivi vya serikali vya utangazaji kuwa chini ya uongozi na uratibu wa menejimenti moja.

Kutokana na nia ya kuongeza kasi ya mabadiliko yaliyokusudiwa ndani ya muda mfupi, na kulifanya Shirika la umma la utangazaji, TUT ilibadilishwa na kuitwa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) kuanzia Julai, 2007. Shirika hili la utangazaji Tanzania lilizinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 26 Machi, 2008.